Select Menu

Slider

Powered by Blogger.

Music

Health

Sports

News

Photos

Documentary

Video

» » STORY ; KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA-5 Miaka mitatu baadaye: Belinda alisoma  kwa mateso bila kumwona Prosper tena, roho yake ilimuuma kila siku na mpaka anamaliza kidato cha sita alikuwa ni mtu wa kumlilia Prosper tu! Wanafunzi wenzake walimcheka,  alipomaliza kidato cha sita alijiunga na Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam kwa masomo ya sheria, mawazo yake yalikuwab bado kwa Prosper! Likizo yake ya kwanza aliamua kusafiri  bila kuwataarifu wazazi wake kwenda  Tabora,  Belinda alidandia treni lililompeleka hadi Tabora mjini ambako alipanda tena basi la Sabena lililokwenda hadi Mbeya, basi hilo lilimshusha kijijini kwao na Prosper Tutuo kilometa kama thelathini kutoka Tabora mjini. Aliingia Tutuo saa saba mchana na kuulizia nyumbani kwa akina Prosper akaonyeshwa, kila mtu kijijini alimshangaa kwa mavazi aliyovaa!   Alishangazwa na hali aliyoikuta nyumbani kwao na Prosper ilikuwa ni nyumba ndogo mno iliyokandikwa kwa udongo na ilianguka upande mmoja. Alipobisha hodi  alipokelewa na mama mmoja aliyevaa nguo zilizochanika na alionekana  kuwa mgonjwa  alikohoa kila baada  ya kuongea sentensi moja! Mama huyo alifanana sana na Prosper. “Karibu binti!” Alisema mama huyo na kumpokea Belinda begi lake na mmoja wa wasichana alilipeleka ndani,  akavuta kigoda kilichokuwa karibu na kumpa Belinda akikalie, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Belinda aliyezaliwa katika familia ya kitajiri kuwa katika familia ya aina ile na alielewa ni kwanini Prosper aliishi maisha duni shuleni. Baada ya salamu Belinda hakusita kueleza sababu ya safari yake! Wasichana   wawili waliovaa magauni yaliyochakaa walikaa pembeni ya mwanamke huyo wakisikiliza. “Mama mimi naitwa Belinda!” “Wewe ndiye Belinda? Uliyeandika barua hapa miaka miwili na nusu iliyopita?” Uliyekuwa ukisoma na prosper Moshi?” Angelina mama  yake Prosper alilipokea jina la Belinda kwa mshangao. “Ndiyo mama na madhumuni ya safari yangu ni kujua aliko Prosper kwa sasa, sababu ni miaka miwili na nusu   sijamwona! Roho inaniuma sana kumpoteza kwani ninampenda!” Badala  ya kujibu ombi la Belinda mama yake Prosper aliangua kilio na hata wasichana waliokaa karibu yake nao walianza kulia machozi. Belinda alishindwa kujizuia na kujikuta nae akilia ingawa hakujua sababu ya wao kulia ilikuwa ni ipi! “Niambieni basi ili nifahamu Prosper yupo wapi hasa?” “Yupo gerezani!” “Alifanya nini Prosper?” “Alimuua baba yake!” Mama yake Prosper alishindwa kuueleza ukweli! Belinda alianguka chini na kuanza kugalagala akilia kwa uchungu   walijaribu kumbembeleza lakini hakusikia, alipotulia swali lake lilikuwa moja tu! “Ni kwanini alimuua baba yake masikini Prosper?” “Unaniona mimi nilivyo mwanangu?” “Ndiyo!” “Sikuzaliwa hivi  unavyoniona yote hii ni kazi ya baba yake prosper, alinitesa sana  kwa kunipiga kila siku na kunitoa viungo vyangu kwa kisu, Prosper alimuua baba yake kwa bahati mbaya akijaribu kunisidia mimi!” Alisema mama huku pia akilia machozi. “Nahitaji kumwona Prosper mama hata huko gerezani mnipeleke!” Alisema Belinda. “Prosper  yupo gereza la Isanga lakini siku ya kumwona ni Jumapili pekee!” Jumapili ilikuwa siku sita mbele yao, Belinda hakuwa na njia nyingine  kumwona Prosper  zaidi ya kusubiri  mpaka siku hiyo ifike! Maisha yalikuwa magumu sana kwake kuendelea kusubiri lakini hakuwa na la kufanya   aliishi nyumbani kwao Prosper akifanya kazi zote za nyumbani na alitumia pesa alizokuwa nazo kutatua baadhi ya matatizo katika familia hiyo. Ni yeye alimpeleka mama yake Prosper hospitali ya Kitete mjini Tabora kupimwa,  daktari aliamua kumpima makohozi, baada ya kuhisi alikuwa na kifua kikuu  na alipigwa  X-ray  ya kifua na kuonekana mapafu yake yalikuwa yameharibika kabisa. Makohozi  yake yalipopimwa kwa muda wa siku tatu yaligungulika  kuwa na wadudu wa  kifua kikuu na kuanzishiwa matibabu!Angelina alimshukuru Belinda kupita kiasi. Siku ya Jumapili ilipofika wote waliondoka kwenda gerezani Isanga, moyo wa Belinda ulikuwa ukidunda kwa nguvu na hakujua nini kingetokea baada ya kukutana na Prosper  alishindwa kupata picha halisi ya Prosper kwa wakati huo lakini aliamini bado alikuwa ni kijana mwenye sura nzuri kama alivyokuwa awali. Walipofika gerezani waliandikisha majini yao na watu waliotaka kuwatembelea, taratibu zote hizo kwa Belinda zilikuwa ni kumchelewesha kumwona Prosper! Baada ya kujiandikisha walionyeshwa  chumba maalum cha kumsubiri Prosper aje na kuongea naye! Dakika kumi   baadaye wakiwa wamekaa, Belinda alishuhudia kijana mmoja mwembamba mrefu akiingia chumbani humo, urefu wake ulikuwa sawa na Prosper lakini  unene wa mwili na ngozi yake  vilikuwa tofauti,alijaa ukurutu mwili mzima! Aliingia  chumba akiongozana na mtu mmoja mwenye mwili mkubwa na ndevu nyingi. Kijana huyo alipotupa macho chumbani akiwaangalia watu waliokuwepo,  ghafla aliruka na kukimbia moja kwa moja kuelekea mahali alipokuwa amekaa Belinda! Alipomfikia ndipo Belinda aligundua kijana huyo alikuwa Prosper lakini katika hali mbaya. “Belinda umefikaje huku?” “Prosper ni wewe? Umekuwaje hivi mpenzi wangu?” Waliangushana  hadi chini na kuanza kulia,  Angelina pamoja na binti zake Nyamizi na Kasanda walishindwa kujizuia na kujikuta wakiangua kilio, mwanaume  aliyeambatana na Prosper    alikwenda  na kumvuta Prosper na kumtoa mikononi mwa Belinda. “Ha! Hebu achianeni!” Alisema mwanaume huyo ambaye baadaye Belinda alimtambua kwa jina la Savimbi. “Kwanini?” Prosper aliuliza. “Kwani huyu msichana ni nani?” “Huyu ni mpenzi wangu!” “Nani amekuambia unatakiwa uwe na mpenzi?” “Savimbi mimi sitakii,niachie bwana niongee na Belinda wangu!” Sura ya Savimbi ilibadilika  na ghafla   bila hata kuuliza alimnyanyua Prosper na kuanza kumvuta kumrudisha ndani ya gereza, Belinda alilia na kushindwa kabisa kuelewa kilichokuwepo  kati ya Savimbi na Prosper  wote walibaki wameangaliana bila kujua la kufanya! **** Belinda hakuamini alichokiona alishangaa ni kwanini mwanaume huyo  amchukue Prosper kabla hajamaliza kiu ya maongezi naye, alifikiria sana na kujikuta akilia. Alishindwa kuelewa ni kitu gani kiliendelea kati ya Prosper na mwanaume aliyemchukua kwa nguvu ukumbini na Prosper alionekana kutokuwa na sauti kabisa mbele ya mwanaume huyo. Kichwa cha Belinda kilihisi kitu fulani lakini hakuwa na uhakika  nacho sana na  alishindwa kupitisha moja kwa moja kuwa kulikuwa na uhusiano wa kishoga kati ya Prosper na mwanaume huyo! “Haiwezekani Prosper ninavyomfahamu hawezi kufanya hivyo!” Aliwaza Belinda! Hapakuwa na sababu ya wao kuendelea kubaki gerezani siku hiyo, walilazimika kuondoka   kwenda hadi stendi   ambako walipanda  basi na kurudi tena kijijini Tutuo! Njiani Belinda  aliwaza mambo mengi sana juu ya kifo cha baba yake Prosper na alishindwa kuelewa ilikuwaje mpaka Prosper akafikia uamuzi huo wa kikatili, mama yake Prosper ilibidi aeleze kila kitu kuhusu ukatili aliofanyiwa na mumewe na hatua aliyoichukua prosper kumkingia mama yake. “kwanini hamkwenda mahakamani mama?” “Mwanamke wa Kinyamwezi hatakiwi kumshtaki mume wake hata kama akipigwa mwanangu!” “Hivi mama yule mwanaume aliyekuja na Prosper pale gerezani ni nani?” “Ni rafiki mkubwa wa Prosper anaitwa Savimbi kila mara tukienda gerezani huwa anakuja naye!” “Mh! Mbona jina lake linatisha?” “Hivyo ndivyo anavyoitwa!” Walifika kijijini saa tisa mchana na Belinda aliendelea kuishi kijijini kwa wiki nyingine zaidi akisubiri Jumapili ifike ili aende gerezani kumwona tena Prosper,  siku ilipofika walikwenda tena gerezani    siku hiyo mama yake Prosper hakwenda kwa sababu hali yake haikuwa nzuri kifua kilimbana sana na alikuwa ameshindwa hata kuhema. Walikwenda Belinda  na dada zake Prosper peke yao na walifanikiwa kuonana na Prosper lakini siku hiyo alikuja peke yake bila Savimbi na kusalimiana nao, dada zake walionekana kushangaa. “Leo Savimbi yupo wapi?” Nyamizi alimuuliza Prosper. “Alipigana na Mnyapara jana!” “Kwanini?” “Kwa sababu Mnyapara alinipa ugali mkubwa na mboga yenye mafuta!” “Ndio wakapigana?” “Ndiyo!” Belinda alizidi kuyaamini mawazo yake, ilikuwa si rahisi watu wapigane sababu ya  Prosper kupewa ugali!Roho ya Belinda iliumia sana na kujikuta akilia alitaka kusema kitu lakini alishindwa sababu dada zake walikuwa pale. “Wifi zangu  mnaweza kunipa nafasi kidogo tu niongee na kaka yenu faragha?” “hakuna shida wifi!” Walijibu na wote wakatoka nje wakiwaacha prosper na Belinda peke yao chumbani, kilikuwa ni chumba chenye mwanga mdogo. “Prosper pamoja na matatizo yote yaliyokupata bado nakupenda!” “Hata mimi nakupenda pia Belinda na sasa ninaamini   hunidanganyi  penzi lako kwangu ni kweli tupu ingawa nasikitika kuwa nitafia gerezani,bila hivyo tungeoana na kuzaa watoto wetu Belinda!” “Usiwe na wasiwasi Prosper bado nina uhakika tutaoana!” “Tutaoanaje wakati mimi tayari nilishahukumiwa kunyongwa?” “Usijali muujiza wa Mungu utatokea na nikirudi nyumbani nitamshawishi baba yangu anipe pesa ili   nikutafutie wakili ajaribu kukutoa gerezani!” “Baba yako atakubali kweli?” “Nina uhakika baba atakubali wala usiwe na wasiwasi mpenzi!” Wote wawili waliangaliana na kujikuta wakitokwa na machozi ya uchungu! Kumbukumbu kubwa sana juu ya maisha yao ilikuja vichwani mwao, mambo mengi waliyoyafanya shuleni na kufurahia maisha yalirejea akilini mwao, Belinda alihisi mapenzi makali sana yakiutwaa tena moyoni mwake! Kweli alimpenda Prosper kuliko kitu kingine chochote, ni wanaume wengi walishamfuata kumtaka mapenzi lakini hakuwakubali moyo wake ulimpenda Prosper kijana masikini  tena aliyekuwa gerezani wakati huo. Kitu kama sumaku kilijitokeza katikati yao na kujikuta wamekumbatiana na kuanza kupapasana miili yao! Kwa mara ya kwanza katika maisha yao tangu wafahamiane walijikuta wakitamaniana kimwili na  mambo yaliyofuata katika muda wa dakika tano ndani ya chumba hicho hayaandikiki wala kuelezeka  ila ilikuwa ni raha ambayo wote wawili waliipata kwa mara ya kwanza maishani mwao. “Proper ahsante! Ninakupenda sana Prosper na sijui nitaishije bila wewe!” Alisema Belinda huku akilia machozi. “Nakupenda pia Belinda  na kama nilivyokueleza bila  haya matatizo tungeoana na kuwa mke na mume!” “Usiwe na wasiwasi Prosper tutaoana tu!” Belinda aliendelea kusisitiza alichokisema awali. “Hivi sasa unasoma wapi?’ “Mimi?” “Ndiyo!” “Baada ya kumaliza kidato cha sita nilijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam ambako ninasoma Sheria!” “Kweli?” “Ndiyo!” “Unataka kuwa mwanasheria Belinda?” “Ndiyo!” “Soma sana uje utusaidie!” Dakika tano baadaye kengele ililia ndani ya gereza na Prosper alinyanyuka na kumkumbatia Belinda walipigana mabusu na kuagana! Mwili wa Prosper ulikuwa  mchafu kupita kiasi  alihisi Belinda angemwonea kinyaa lakini haikuwa hivyo, Belinda hakujali wala kuonyesha kushangazwa na hali hiyo alizidi kumkumbatia. “Belinda ni lazima niende sasa muda wa kuongea na wewe umekwisha!” “Sawa darling lakini jaribu kuwa mwangalifu sana na Savimbi siipendi tabia yake!” Prosper hakujibu kitu alizidi kuinamisha kichwa chake chini kwa aibu jambo lililomfanya Belinda aendelee kupata uhakika kuwa kulikuwa na jambo kati yao! Baada ya kuagana Belinda alitoka nje ya gereza na kuungana na wifi zake na safari ya kwenda stendi kupanda basi la kuwarudisha nyumbani ilianza, njia nzima Belinda alikuwa ni mwenye mawazo  alifika akiwa amechoka na kujitupa kitandani ambako aliendelea kumlilia Prosper!               ***************   Alikaa Tabora kwa wiki tatu  bila wazazi wake kufahamu mahali alikokuwa, baba mzazi yake alishamtafuta kila mahali  bila kumpata mpaka kukata tamaa! Alitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari lakini bado hakufanikiwa kumpata binti yake, wengi walihisi Belinda alikufa lakini baba yake hakuliamini hilo. Hatimaye mzee Thomson Komba baba yake Belinda aliamua kutangaza zawadi nono ya shilingi milioni kumi kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwa Belinda,  wanakijiji wawili wa kijiji cha Tutuo walijitokeza na kwenda kutoa taarifa moja kwa moja kituo cha polisi Belinda akawa amekamatwa. Siku aliyokamatwa aliiacha familia  ya akina Prosper katika majonzi makubwa kwa sababu kwao mkombozi alikuwa ameondoka! Kukaa kwa Belinda katika familia hiyo kulipunguza sana shida zao za maisha, pesa yote aliyokuwa nayo aliitumia katika matumizi ya nyumbani na ni yeye pia aliyenunua dawa za mama yake Prosper. Alichokifanya Belinda wakati wa kuondoka ni  kumtupia Nyamizi dada yake Prosper shilingi elfu hamsini alizokuwa nazo katika mfuko wa suruali ili  ziwasaidie. “Wifi!Pesa hizo zitawasaidia!” “Ahsante wifi, ahsante kwa kuja tafadhali utukumbuke!” “Sawa wifi! Muangalieni sana mama sababu hali yake si nzuri!”             ***************** Belinda alichukuliwa kwa nguvu na kupakiwa ndani ya gari lililompeleka hadi Tabora ambako alisafirishwa kwa ndege ya kukodi hadi Dar es Salaam, alipokelewa na kupelekwa moja kwa moja   kituo cha polisi ambako aliwekwa rumande na kukaa kwa  siku tatu, alipotolewa aliendelea na adhabu nyingine kali  nyumbani kwao. Pamoja na adhabu hizo bado Belinda hakuwa tayari kueleza ukweli juu ya mahali alikokuwa, aliendelea kudanganya kuwa alikwenda kwao na rafiki yake msichana waliyesoma naye darasa moja! “Bila kuaga?” “Nisamehe baba!” Na kweli Belinda alisamehewa  na kuendelea na maisha kama kawaida nyumbani kwao lakini mawazo yake yote yalikuwa kwa Prosper aliyekuwa bado yupo gerezani, alimlilia na alishindwa kula kwa sababu yake! Alitamani kuwa na Prosper tena na hakujua kama katika maisha yake angeweza kumpenda mwanaume mwingine kama alivyompenda Prosper. Belinda alikonda kwa mawazo na baba yake alimshangaa kwa mabadiliko ya afya ya mwili wake, hakuijua sababu ya tatizo hilo, alijitahidi kumpa mtoto wake kila alichotaka kama njia ya kumbembeleza akiamini  Belinda alichukizwa na adhabu alizompa. Chuo kilipofunguliwa wiki mbili baadaye Belinda alirudi tena Mlimani na kuendelea na masomo yake ya Sheria lakini kitabu kikawa kigumu kwake kwani kila alipomfikiria Prosper akili yake ilizidi kuchanganyika na kupoteza pointi. Kitu kingine kilichomshangaza zaidi ni mabadiliko ya hali yake ya afya, alianza kujisikia mchovu kupita kiasi hasa nyakati za asubuhi, uchovu ulioambatana na kichefuchefu na alitapika sana asubuhi, matiti yake yalianza kuvimba! Mwanzoni alifikiri ni malaria lakini alipokwenda kupimwa damu yake ilikuwa safi. Hali yake iliendelea kuwa mbaya na alipitiliza mwezi mmoja katika mpangilio wake wa hedhi! Hilo ndilo lilimchanganya zaidi hatimaye  akaamua kupimwa kila kitu ndipo alipogundua kumbe alikuwa tayari ni mjamzito wa mwezi mmoja na nusu! Belinda alichanganyikiwa, alishindwa kuelewa angemwambia nini mzee Thomson! Kila alipoufikiria ukali wa baba yake alizidi kuingiwa na hofu, alijua mzee yule angemuua,  asingemwacha hai hata kidogo kwani hayo ndiyo yalikuwa maongezi yake ya kila siku. “Mtoto wangu akipata mimba ni lazima nimpige risasi!” Kila alipoikumbuka kauli hiyo ya baba yake alitetemeka mwili  na hakujua ni kitu gani angefanya ili kujiepusha na hasira ya mzazi wake, alipoomba ushauri kwa rafiki zake walimwambia afanye kila alichoweza ili aitoe mimba hiyo kabla mambo hayajaharibika na mimba kuwa kubwa zaidi. Jambo hilo lilimshinda Belinda, alikuwa na uhakika kabisa Prosper angenyongwa na asingemwona tena, alipenda abaki na ukumbusho wa Prosper mwanaume aliyempenda kuliko wanaume wengine wote duniani na ukumbusho pekee ulikuwa ni mtoto na Mungu alikuwa amelikubali hilo. “Siwezi kuua mtoto wa Prosper lolote litakalokuwa na liwe!” Alisema Belinda. Alivumilia na mimba yake chuoni mpaka ikafikisha miezi minne akawa haendi tena nyumbani kwao kila mwisho wa wiki, jambo lililowashtua ndugu zake na kuwafanya kaka zake waende shuleni kumuuliza lipi lilikuwa likimsumbua. Ni hao ndio waliomgundua Belinda na mimba yake na bila hata kusita walizipeleka taarifa moja kwa moja kwa mzee Thomson! Belinda alihisi hilo lingetokea ni asubuhi ya siku iliyofuata tu alipopanda basi  kwenda Tabora nyumbani kwao na Prosper kujificha mpaka azae mtoto wake.                       ****************** Belinda aliingia Tabora jioni ya saa kumi akiwa amechoka hoi bin taaban, hakutaka kupoteza muda hata kidogo mjini alipanda basi la mwisho kumpeleka hadi kijijini Tutuo! Hakuwa na mzigo mwingine zaidi ya begi lililojaa nguo zake mwenyewe, hakuwa na pesa zaidi ya shilingi elfu kumi aliyokuwa amebakiza. Alijua wazi kuwa alikokuwa anakwenda kulikuwa na taabu kubwa na nzito ikimsubiri, alijua tangu siku hiyo asingepata msaada wowote kutoka kwa baba yake  sababu alikuwa amemuudhi kupita kiasi! Isitoshe alijua wazi kuwa mama yake wa kambo na ndugu zake wangemjaza chuki baba yake ili azidi kumchukia. “Lolote na liwe lakini  sipo tayari  kumuua mtoto wangu! Ni bora mimi niteseke lakini kiumbe hiki kizaliwe kama ni masomo nitaendelea nayo baadaye ingawa sina uhakika ni nani atanilipia ada!” Aliwaza Belinda wakati akitembea kuelekea nyumbani kwao na Prosper. Alishangazwa na umati mkubwa wa watu aliouona alipokaribia nyumba yao, wanaume wengi walikuwa wamekaa katika miduara wakiota moto na wengine walionekana kula chakula! Belinda alishindwa kuelewa ni nini kilikuwa kimetokea. Alipofika kwenye uwanja wa nyumba alishangaa kuwaona wifi zake wakija mbio huku wakilia machozi! Wote walimkumbatia huku wakimtaarifa kuwa mama yao alikuwa amefariki asubuhi ya siku hiyo. “Mama amefariki leo! Na hapa tulipo hata pesa ya sanda tumekosa!” Nyamizi alimwambia Belinda baada ya kuketi chini huku akilia na kujifuta machozi. “Ni heri umekufa wifi maana hapa ndani hatuna hata senti, nafikiri utatusaidia pesa kidogo tukanunue sanda na kuchonga jeneza!” Belinda alipofikiria pesa aliyokuwa nayo mfukoni ilikuwa ni shilingi elfu kumi peke yake, hiyo ndiyo ilikuwa maisha  yake hakuwa na tegemeo la  kupata pesa mahali pengine mpaka wakati wa kujifungua! Hakuwa na jinsi ilikuwa ni lazima asaidie, alichukua pochi yake  na kuifungua akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi Nyamizi ambaye naye aliwakabidhi wazee wa kijiji ili waende kununua sanda. Huo ndio ulikuwa mwisho wa Belinda kuwa na pesa, alielewa mbele kulikuwa na shida kubwa kwa sababu nyumbani kwao na prosper asingeweza kupata msaada wowote! Pamoja na hayo yote hakuwa tayari kumuua mtoto wake. Je nini kitaendelea? Tukutane Jumatano Unaweza kushare kwa ajili ya marafiki zako.

About Arusha99

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments

Leave a Reply