HIVI ndivyo anavyosema mkulima wa nyanya kutoka katika kijiji cha Mangalali, bwana Paschal Sichalwe baada ya kuanza kubadili mbinu za kilimo za kizamani na kuanza kutumia mbinu za kisasa alizozipata kupitia mafunzo yanayotolewa na mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI)
http://pagead2.googlesyndication.com/pagead/js/adsbygoogle.js
Mjasiriamali huyu mdogo anaelezea namna ambavyo mradi wa MUVI ulivyoonesha njia ya kuelekea kwenye mafanikio kwa kutoa mafunzo ya kilimo bora, kuboresha njia za mawasiliano baina yao pia jitihada zinazofanywa katika kuwaunganisha na masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi Mradi wa MUVI kwa kushirikiana na viongozi wa shirikisho la wakulima wa nyanya wamefanya ziara za ndani na nje ya nchi katika harakati za kutafuta masoko zaidi, katika hatua za awali uongozi huo umefika nchini Kenya, Malawi na hatimaye Zambia hii ikiwa ni kwa upande wa masoko ya nje Masoko ya ndani, mradi wa MUVI ambao pia umeimarisha kitengo chake cha biashara na masoko wameangalia masoko ya ndani ya nchini na kugundua kuwa kinachosababisha nyanya kushuka bei ni kukosekana kwa taarifa za biashara na masoko kutoka katika ngazi zote. Katika kutatua tatizo hilo tayari mtandao wa mawasilano kutoka mikoa yote Tanzania zitakuwa zikipatikana ili wazalishaji wa nyanya waweze kufahamu soko liliko. Wakulima wanapopata taarifa za biashara na masoko inakuwa rahisi kwao kufanya maamuzi ya soko. Pia matumizi ya mbao za matangazo kwa kushirikiana na redio country fm88.5 fm na Uplands redio 89.0 fm wajasiriamali vijijini wataweza kupata taarifa za biashara na masoko. Aidha bwana Sichalwe ambaye ameanza kuvuna nyanya alizopanda kitaalamu akitumia mbegu bora aina ya Eden inayozalishwa na Kampuni ya Monsanto anasema kuwa ameanza kuona faida kwani mara ya kwanza ameweza kuchuma tenga 33 ilihali msimu mzima uliopita katika shamba hilo hilo lenye ukubwa wa nusu ekari kwa ujumla alivuna kiasi cha tenga 56 tu. “Msimu uliopita nilitumia mbegu aina ya ONXL katika shamba la nusu ekari michumo yote nilipata tenga 56 tu lakini sasa mchumo mmoja nimewezakuchuma tenga 33 na nategemea kuchuma kiasi cha tenga 26 katika mchumo wa pili.” anasisistiza Sichalwe. Msimu uliopita nilitumia kiasi cha shilingi 532,800 ikiwa ni gharama nzima ya uzalishaji kwa upande wa pembejeo pamoja na nguvukazi,mapato ilikuwa 606000, msimu huu nimetumia kiasi cha shilingi 570,900 kwa ajili ya pembejeo na nguvu kazi nategemea kupata kiasi cha shilingi 1,045,000 Kwa mtizamo wa haraka haraka, bwana Sichalwe ameanza kuona faida katika kilimo cha nyanya kufuatia mchanganuo huo alioufanya. Sichalwe ambaye pia pamoja na zao la nyanya hujishughulisha na kilimo cha alizeti na mahindi, katika hatua nyingine amewezakuimarisha biashara ya kuuza bidhaa ndogondogo kwenye kibanda chake ambapo pia anaamini kuwa kuna siku atakuwa mjasiriamali mkubwa. Awali Sichalwe alikuwa akilima kwa mazoea bila kutunza kumbukumbu kuanzia uzalishaji hadi sokoni lakini baada ya mradi wa MUVI kupisha hodi kijijini kwake na kufundishwa kilimo cha kibiashara na njia rahisi ya kuandaa mpango biashara sasa ameweza kutunza taarifa zake za kilimo tangu hatua ya mwanzo hadi mwisho, hapo ndipo anapoweza kubaini mapato na matumizi katika shughuli nzima. “Wajasiriamali wengi wanasahau kuweka kumbukumbu za uzalisha katika shuguli zao wanazofanya kila siku, mali bila daftari hupotea bila kujua,kila unachofanya inakupasa uandike, kuna wengine pia hujisahau wao wenyewe, mfano akipalilia nyanya mwenyewe au akipanda hujisahau katika kipengele cha malipo ile ni nguvu kazi inapaswa kulipwa na hili linawezekana kama utakuwa umeandika”anasema. Katika hatua nyingine Sichalwe anaamini kuwa baada ya kupata mavuno mengi na yakutosha msimu huu anatarajia kuanza kilimo cha umwagiliaji ambacho anaamini kuwa kitamkomboa zaidi. Pamoja na mambo mengine Sichalwe anampango wa kuimarisha kilimo cha ufugaji kwani tayari amenunua mbuzi 5 mara baada ya kuuza nyanya. Idadi hiyo anaona kuwa haitoshi hivyo anategemea kuongeza kiasi hicho hadi kufikia mbuzi 20. Si hapo tu Sichalwe anaamini pia kwa kuzingatia mbinu za kisasa alizozipata kupitia mradi wa MUVI kufikia mwishoni mwa mwaka atakuwa amenza ujenzi wa nyumba ya kisasa ya kuishi. Katika kuhakikisha kuwa Sichalwe na wajasiriamali wengine wanaozalisha nyanya kijijini hapo wanapata mafanikio, mradi wa MUVI umemtuma ofisa masoko wa mradi huo kuzungumza na na wakulima wa nyanya katika hali ya kuwaondoa hofu hususani kwenye kipengele cha masoko. Akizungumza na wajasiriamali wa Mangalali hivi karibuni muda mfupi mara baada ya kuunda kamati ya biashara na masoko, Ofisa masoko wa mradi, bwana Fredy Mumbuli amesema, wakulima wanategemea zaidi soko la Kariakoo na Ilala.Wafanyabiashara hawa huwa wanakimbilia katika masoko haya kwa kukosa taarifa nzuri za masoko. “wajasiriamali hupeleka nyanya kwa wingi katika masoko hayo kwa kukosa taarifa sahihi za masoko hali inayoplekea kushuka kwa bei ya bidhaa husika,wakulima wote nchini wakishavuna hufikiria kuuza bidhaa zao Dar es salaam jambo ambalo si sahihi hata kidogo.”alisema Mumbuli. na kuzidi kubainisha kwamba kuwa kuna wakati kunakuwepo na uhitaji mkubwa wa nyanya Morogogo, Arusha au Dodoma na hata wakati mwingine Iringa Mkulima anayezalisha nyanya Morogoro akipata taarifa za soko zuri la nyanya Iringa anaruhusiwa kufanya biashara vivyo hivyo na kwa upande wa mkulima wa Arusha, Kilimanjaro na mikoa mingine inayolima zao hilo. Hili litawezekana mara baada ya kuimarisha njia za upashanaji habari kupitia vyombo vya habari na mbao za matangazo ambazo tayari mradi wa MUVI umejenga katika kata 16 mkoani Iringa na Njombe. Kitengo cha habari na mawasiliano kitakuwa kikifanya kazi kwa ushirikiano mzuri na kitengo cha biashara na masoko katika kuwapatia wakulima taarifa za biashara na masoko.
No comments